Jumamosi 1 Novemba 2025 - 16:14
Daima ujihesabu kuwa ni mwenye kukosea

Hawza/ Kuyakuza matendo yako mema na kudharau dhambi au makosa yako, kunaweza kuwa kizuizi kikubwa katika njia ya uchamungu wa kweli. Ndiyo maana mafundisho ya Maimamu watoharifu (as) katika jambo hili ni mwongozo wenye thamani kubwa.

Shirika la Habari la Hawza – Imam Zayn al-‘Abidin (a.s.) anamsemesha Mwenyezi Mungu kwa maneno haya:

«اللَّهُمَّ ... أَلْبِسْنِی زِینَةَ الْمُتَّقِینَ، فِی ... اسْتِقْلَالِ الْخَیرِ وَ إِنْ کثُرَ مِنْ قَوْلِی وَ فِعْلِی، وَ اسْتِکثَارِ الشَّرِّ وَ إِنْ قَلَّ مِنْ قَوْلِی وَ فِعْلِی.»

Ee Mungu! Nivishe vazi la mapambo ya wachamungu katika kujihesabu kuwa nimefanya kheri kidogo, hata kama matendo yangu ni mengi, na kuiona shari kuwa kubwa, hata kama imenipata kidogo, iwe katika maneno au matendo yangu. (1)

Sherehe:
Jambo ambalo linaweza kuwa kama janga linaloharibu kila hazina ya kiroho kwa mwanadamu katika njia ya uchaji, na kumfanya asimame au hata arudi nyuma katika safari yake ya kumuabudu Mwenyezi Mungu, ni pale mtu anapoyaona matendo yake mema kuwa makubwa, huku akiudharau na kupuuza makosa na udhaifu wake.

Iwapo tutaiona dunia yote kuwa ni mbele ya uwepo wa Mwenyezi Mungu, na tukajihisi kila wakati tupo katika hadhara Yake, na tukatambua kwamba Yeye ndiye mmiliki wa kila kitu tulicho nacho, basi kamwe hatutaangukia katika maradhi haya ya kiroho.

Imam Musa al-Kadhim (a.s.) alimnasihi mwanawe kwa kusema:

«یَا بُنَیَّ عَلَیْکَ بِالْجِدِّ لاَ تُخْرِجَنَّ نَفْسَکَ مِنْ حَدِّ اَلتَّقْصِیرِ فِی عِبَادَةِ اَللَّهِ عَزَّ وَجَلَّ وَطَاعَتِهِ فَإِنَّ اَللَّهَ لاَ یُعْبَدُ حَقَّ عِبَادَتِهِ.»

Ewe mwanangu! Jitahidi kwa bidii, na usijione kuwa umetimiza haki ya ibada na utiifu kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwani Mwenyezi Mungu hawezi kuabudiwa kwa kiwango anachostahiki. (2)

Imam Ja‘far al-Sadiq (a.s.) naye ametuhimiza kwa maneno haya:

«أَکْثِرْ مِنْ أَنْ تَقُولَ ... لاَ تُخْرِجْنِی مِنَ اَلتَّقْصِیرِ.»

Kithirisheni kusema: Ee Mola wangu! Usiniondoe katika hali ya kujihesabu kuwa nimekosea kutosha.

Walipomuuliza kuhusu maana ya kauli hiyo, Imam akajibu:

«کُلُّ عَمَلٍ تُرِیدُ بِهِ اَللَّهَ عَزَّ وَ جَلَّ فَکُنْ فِیهِ مُقَصِّراً عِنْدَ نَفْسِکَ فَإِنَّ اَلنَّاسَ کُلَّهُمْ فِی أَعْمَالِهِم فِیمَا بَیْنَهُمْ وَ بَیْنَ اَللَّهِ مُقَصِّرُونَ.»

Kila amali unayoitenda kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, jione kwamba hujalitimiza ipasavyo, kwa sababu watu wote katika matendo yao baina yao na Mwenyezi Mungu ni wenye mapungufu. (3)

Rejea:
1- Sahifa Sajjadiyya, Dua ya 20 – Makarim al-Akhlaq
2- Wasā’il al-Shī‘a, juzuu ya 1, uk. 95
3- Usūl al-Kāfī, juzuu ya 2, uk. 73

Imetayarishwa na Idara ya Elimu na Utamaduni ya Shirika la Habari la Hawza.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha